Yapata wiki tatu sasa tangu msanii mwenzangu Steven Kanumba aage
dunia, na kama ilivyo kwa kila kitu kinapotokea huandamana na kila aina
ya maneno na hisia mbali mbali kutokana na mitazamo ya watu kupishana
kuhusiana na jambo husika. Kulingana na muktadha huo, msiba wa Steven Kanumba
umekumbwa na maneno na hisia kama hizo,hususan mazingira ya kifo chake;
kinachosikitisha zaidi watu wengi (ambao wanajitambulisha kama wapenzi
wa Kanumba), na baadhi ya vyombo binafsi vya habari vimekuwa
vikinihusisha na kifo hicho, kwa kusema kwamba kwa njia moja au nyingine
ninahusika na mauaji ya Steven Kanumba.
Kwa muda wote huo tangu msiba ulipotokea mpaka leo hii nashika
kalamu kujaribu kuyaweka sawa na kuondosha hisia chafu katika fikra za
watu, nimekuwa nikipitia katika wakati mgumu sana kwa jinsi ambavyo
nimekuwa nikinyooshewa vidole kila upande nikihusishwa na kifo hicho,
kiujumla nimezingatia maoni ya wapenzi ya mashabiki wangu wakinitaka
kuwa na subira, ila kuna ukweli usemao kwamba, uongo ukirudiwa sana
jamii huusadiki na kuuona ukweli,nimeona nisikae kimya ila niweke sawa
hili kwamba sihusiki na kifo cha Steven Kanumba.
Nasema wazi kwanza sihusiki kabisa na kifo cha Kanumba kwanza kwa
kuzingatia mazingira yenyewe ya kifo kilivyotokea. Wakati kifo hicho
kinatokea, nilikuwa sehemu nyingine kabisa na mimi nilikuwa mtu wa tatu
kutaarifiwa kwamba Kanumba amepatwa na mkasa ambao baadae ulisababisha
kifo chake. Na na hata nilipofika katika hospitali ya Muhimbili (tofauti
na watu wanavyodhani kuwa nilifika nyumbani kwake; ukweli mimi
nilimkuta tayari amepelekwa Muhimbili), nilikuta tayari alikuwa
ameshafariki ndio maana hata Polisi wanaohusika na usalama wa raia, si
tu kwamba hawakuniweka chini ya ulinzi, sikuitwa hata kuhojiwa kwa
sababu hakuna mazingira yoyote yanayonihusisha mimi na kifo hicho.
Pili, watu wanahusisha tofauti za kibinadamu zilizokuwepo baina yetu
na kifo hicho, nasema hii sio sahihi kwa sababu kwanza ni kawaida kwa
binadamu kutofautiana,isipokuwa kwetu sisi baadhi ya vyombo vya habari
vilikuwa vinakuza kwa sababu nisizozijua, hivyo jamii ikachukulia kuwa
tofauti zile ni uadui kitu ambacho sio sahihi, kwani sisi hatukuwa watu
pekee tunaotofautiana kwani huu ni mwenendo wa kawaida wa dunia; hivi
jana tumeshuhudia Waziri mmoja akieleza bayana katika mkutano na
waandishi wa habari kuwa na tofauti na naibu wake, lakini hatuajasikia
ikiandikwa wana ‘bifu’ bali imetafutwa lugha nzuri ya kupamba tofauti
hizo, kwa kuwa waliohusika ni waheshimiwa, ila kwa wengine kutokana na
sababu tusizozijua, inaonekana kama ni haki yetu kuandikwa vibaya.
Kinachosikitisha, kwa nini jambo hili linachukuliwa kwa mkazo mkubwa
sana, kwani hatujawahi kusikia watu wakiwa wanatofautiana na ndugu jamaa
hata na marafiki zao na inaonekana kawaida tu? Kwani vyombo vya habari
havikuwahi kuandika kuwa marehemu Steven Kanumba alikuwa na tofauti na
baba yake, na yeye mwenyewe alitamka hivyo katika vyombo vya habari,
mbona wameliongea bila kuongeza chumvi, na jamii inaona kuwa ni jambo la
kawaida la kibinadamu.
Pengine watu wanaojaribu kuongea hayo, hawajui mimi na Steven Kanumba tumetoka
wapi? Sisi si watu tuliokutana barabarani, tuna historia katika kazi
yetu ya sanaa na pia katika maisha maisha yetu. Mwanzoni kabisa, mimi
ndiye niliyempokea Kanumba pale Kaole na ndiye niliyemfundisha sanaa
pale (nadhani watu wanakumbuka tamthiliya za wakati huo ITV) na baada ya
hapo tulienda pamoja katika kampuni ya Game 1st Quality pamoja na tukafanya filamu kama Johari, ‘Sikitiko Langu’, ‘Dangerous Desire’ na nyinginezo, na tuliendelea kuwa pamoja katika kampuni hiyo mpaka tulipofanya filamu ya ‘Oprah’ mwaka
2008 ambapo niliingia rasmi kufanya kazi za kampuni yangu, lakini
tuliendelea kuwa pamoja hata wakati nikiendelea na kazi za kampuni
yangu.
Pia mimi nilikuwa wa kwanza kuanza kufanya kazi na Steps na baadae
Kanumba alipoanza kufanya kazi zake mwenyewe na kunikuta huko
tuliendelea kuwa pamoja kama siku zote. Kitu kikubwa kilichokuwa
kinaendelea baina yetu, ni kwamba tulijenga ushindani wa kuendeleza kazi
mbele kwa kila mmoja akitoa kazi, mwingine anamjibu.
Isitoshe hata vitu vyetu binafsi utaona kama kuna kufanana; kuna
wakati Kanumba alinunua Toyota Ruv 4 nyeusi mimi nikanunua ya kijani,
aliponunua Harrier na mimi nikanunua pia, na hata gari za hivi karibuni,
ukitazama utaona kuwa zinafana kwa karibu; hii ilikuwa ni kama maisha
yetu, hatukuwa na uadui, ilikuwa tunapeana changamoto za maendeleo.
Watu wanaojaribu kuonesha kuwa tofauti zetu ilikuwa ni uadui, huwa
hawajui wapi tulikotoka ndio maana wanasema wasemavyo na katika
kuthibitisha kuwa tofauti hizo hazikufikia katika uadui, kuna watu ambao
wanafanya kazi nami katika kampuni yangu ya RJ ndio hao hao Kanumba
alikuwa anawatumia siku zote katika kazi zake, hata baada ya tofauti
hizo hakuna aliyekoma kufanya kazi na yeyote kati yetu.
Hii inathibitisha kuwa tofauti ilikuwa kati yetu kama binadamu, sio chuki za kimafanikio, ingekuwa hivyo watu kama Junior Syaary ambaye mara nyingi hufanya final editing katika RJ ndio huyo huyo alikuwa akifanya na Kanumba, Ally Yakuti ambaye anaandika script za RJ, ndiye huyo huyo aliyekuwa anaandika kwa Kanumba, Steven Shoo ambaye ni mtaalamu wangu wa light, ndiye huyo huyo anayetumiwa na Kanumba na wengine wengi kama Juma Chikoka aliyecheza kikamilifu katika filamu ya ‘Kijiji cha Tambua Haki’,
ambaye pia anashiriki filamu nyingi za RJ, na wote hao, hawakuanzia kwa
Kanumba, wote wameanza kwangu mimi ndio niliompatia na hata baada ya
hayo yanayosemwa kuwa kuwa ni uadui, sikuwahi kuwakataza kufanya kazi na
Kanumba.
Tatu kumtuhumu mtu kwa namna yoyote ile bila ya uthibitisho wa
tuhuma hizo, ni kosa kwa sheria za nchi na pia kama ni mfuasi wa dini
yoyote ni dhambi, kwani wakati ukisema hayo huku hujui uhalisia bali
unasukumwa na nguvu za hisia tu ni sawa na kumchafua mtu huyo katika
jamii bila ya kujua jamii inamchukuliaje. Napenda kusema wazi wazi kuwa,
kwa kila anayetekwa na wimbi hili, ajaribu kufikiria leo ipo kwangu
mimi, kesho inaweza kuhamia kwako, kwani mimi sio wa kwanza kufikwa na
haya, inaweza kukukuta hata wewe au ndugu yako, utajisikiaje.
Na kama kweli mimi nimehusika na kifo cha Kanumba kwa namna yoyote
ile, basi Mungu atanihukumu na kila aliye hai atashuhudia, ila kama
sijahusika kwa lolote, Mungu hatonihukumu na badala yake ataniinua, kwa
kuwa ninapita katika kipindi kigumu mno sasa hivi kwa madhila haya.
Mwisho kabisa napenda kumaliza kwa msemo usemao, ajidhaniaye
amesimama, aangalie asianguke, kwani kadri mambo haya yanavyoendelea,
usidhani yataishia kwangu, kwani mkono wa dhuluma haushii karibu,
ukisikia jirani anapiga kelele za mwizi, usilale kamsaidie, usiseme kuwa
hatuhusiki kwani hayupo kwetu, kesho utafikwa na wewe utakosa wa
kukusaidia. cha msingi kama tunampenda sana ndugu yetu ni kumuombea kwa
Mungu, kwani hatujui makao yake huko aliko, na sio kuunda vitu ambavyo
kamwe hata yeye angekuwa hai asingeviafiki.”
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU STEVEN KANUMBA MAHALI PEMA PEPONI.
MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA. |
No comments:
Post a Comment